Na. Haruna Taratibu
Shirika lisilo la Kiserikali la World Vision Tanzania kupitia Mradi wake wa Kanadi wilayani Itilima limeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya tano za kupambana na kutokomeza Malaria katika jamii ya Wanaitilima Mkoani Simiyu kwa kutoa vyandaruwa kwa watoto 6,160.
Zoezi hilo la utoaji wa vyandaruwa vyenye viuatilifu vinavyodumu muda mrefu lilifanyika kwa watoto wafadhiliwa 3,431 na wasio wafadhiliwa 2,729 kwa ujumla wao wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi.
Akiongea katika hafla ya kukabidhi vyandaruwa hivyo Mratibu wa Mradi kutoka World Vision Ndg. Nyamoko George amesema kuwa Shirika hilo katika Miradi yake yote limejikita katika kuhakikisha watoto wanapata ustawi katika Nyanja zote za elimu, Afya, na Usalama na haki zao.
“tunaamini kwa vyandarua hivi , maambukizi ya Malaria yatapungua kama si kuisha kabisa, tukizingatia Mpango Mkakati wa Wizara (NMCP) ni kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria Kutoka asilimia 7 hadi chini ya asillima moja ifikapo mwaka 2020 na kuitokomeza kabisa malaria ifikapo 2030” alisema Ndg. Nyamoko
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itilima Dkt. Anold Msiba amesema kuwa Malaria bado ni ugonjwa unaosumbua Wananchi Wilayani Itilima na takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi kwa wilaya ni asilima 5.1.
“Hata hivyo Halmashauri imekuwa ikishirikiana na Wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwa pamoja na kuelimisha wananchi kufuata kanuni na njia mbalimbali za kujikinga na Malaria kwa kutumia vyandaruwa vyenye Viuatilifu vya muda mrefu sambamba na upuliziaji viuadudu vya Ki-baiolojia kwenye maeneo yenye mazalia ya mbu na kutoa tiba kinga kwa Mama wajawazito” amesema Dkt. Msiba
Akikabidhi vyandaruwa hivyo kwa walengwa kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mhe. Benson Kilangi, Katibu Tawala wa Wilaya Ndg. Filbert Kanyirizu aliwaasa Wazazi na Walezi wa Watoto hao kutumia vyandaruwa hivyo kama ilivyo kusudiwa na kuhakikisha wanawahi haraka katika vituo vya kutolea huduma za Afya pindi wanapo hisi dalili za ugonjwa wa malaria.
Wilaya ya Itilima katika mapambano dhidi ya Malaria imekua ikishirikiana na Wadau mbalimbali wakiongozwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria, World Vision Tanzania, USAID Boresha Afya, AMREF, TMARC, Johns Hoppkins University, PSI na Chama cha Msalaba mwekundu Tanzania (TRCS) wadau hawa kwanamna moja ama nyingine wamehuisha lengo la serikali la kutokomeza Ugonjwa wa Malaria nchini ifikapo mwaka 2030 lenye kaulimbiu ya “ZIRO MALARIA INANZA NA MIMI” .
DED - ITILIMA
Sanduku la Posta: 308 BARIADI
Simu: +255 28 29 863 29
Simu: 028 29 863 28
Barua Pepe: info@itilimadc.go.tz
Hatimiliki ©2016 Kitengo cha TEHAMA. Haki Zote Zimehifadhiwa