KULETA SIKU YA UHIMILISHAJI KITAIFA WILAYANI ITILIMA
UJENZI WA MAJOSHO MATATU KATIKA BAJETI IJAYO YA WIZARA YA MIFUGO
VIJIJI VILIVYO KANDOKANDO MWA HIFADHI KUCHUNGA NDANI YA MITA 500
Waziri wa mifugo na uvuvi Mhe. Luhaga Mpina ameahadi kuleta kampeni ya kitaifa ya uhimilishaji wa mbegu bora ya Mifugo wilayani Itilima ambapo huduma hiyo itatolewa bure kwa ng’ombe 1,000/ na baada ya hapo zoezi hili litafanyika kwa Tsh. 10,000/ kwa ng’ombe badala ya Tsh. 30,000/ bei ya awali.
Akiongea na Wafugaji Wilayani Itilima Mhe. Mpina alisema“Serikali ya awamu ya tano inayo ongozwa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli imekusudia kuimarisha sekta ya mifugo ili kwenda sambamba na uchumi wa viwanda na ndiyo maana Serikali hii imejenga machinjio bora na za kisasa katika baadhi ya mikoa nchini Ikiwemo machinjio ya Dar es Salaam yenye uwezo wa kuchinja Ng’ombe 1000 kwa siku na Viwanda vya kuchakata malighafi mbalimbali zitokanazo na Mifugo”
Aidha Mhe. Mpina alisema ya kwamba uwepo wa machinjio hizi utaenda sambamba na mabadiliko makubwa katika sekta nzima ya mifugo ikiwemo uboreshaji wa Miundombinu yote inayo hitajika majosho, upatikanaji wa madawa sahihi ya Mifugo, pamoja na kufanya uhimilishaji wa mbegu bora ili kuwa na mifugo yenye afya na ya kisasa.
Mhe. Mpina aliongeza ya kuwa “Mhe. Rais Magufuli kwa kutambua umuhimu wa sekta ya Mifugo amefuta pendekezo la kuhamisha vijiji 920 vya Wafugaji vilivyopo ndani ya mita 500, kutoka eneo la mpaka wa hifadhi mbalimbali nchini na kipindi cha kiangazi eneo hilo la mita 500 litatumika kwa malisho ya mifugo, kwa upande wa Itilima, vijiji vilivyopo katika orodha hiyo ni Mwaswale, ng’walali, Nyantugutu, Mwamakili, Mbogo, Pijulu, Shishani , Longalombogo na Ndingho ”.
Sanjari na hayo, Mhe. Mpina alisisitiza kwa wafugaji kuhakikisha wanaogesha mifugo yao kila inapo hitajika “ kwani magonjwa mengi ya mifugo yanatokana na kupe, tukijikita kikamilifu katika uogeshaji tutaweza kuokoa mifugo mingi sana na katika kufanikisha zoezi hili Serikali kupitia ruzuku ya dawa ya kuogeshea mifugo inayo tolewa kila baada ya miezi sita, sasa mfugaji ataogesha Ngo’mbe mmoja kwa Tsh. 50 na mbuzi au kondoo wataoga kwa Tsh. 10” alisema Mhe. Mpina.
Ili kufikia malengo hayo Waziri. Mpina alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Bi. Elizabeth M. Gumbo kuhakikisha ukarabati wa majosho ambayo hayatoi huduma za uogeshaji unafanyika na Kupitia Wizara ya Mifugo watakarabati Majosho matatu.
Baada ya kuuliza changamoto zinazo wakabili Wafugaji, lilijitokeza suala la wafugaji walio taifishiwa mifugo yao (ng’ombe) 336 na Mamlaka ya Hifadhi ya Poli la Akiba la Maswa mwaka 2017, lililo wasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa jumuhiya ya Wafugaji Wilayani Itilima Ndg. John Ludeya na kutiliwa mkazo na Ndg. Alex Mageme Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Itilima.
Bw. Ludeya alisema yakwamba mifugo 336 iliyo taifishwa ilikutwa ikichunga katika maeneo ya kandokando mwa Hifadhi hiyo, lakini mapema mwaka huu (2020) wafugaji hao kwa idhini ya mahama iliamuliwa warudishiwe Mifugo yao na mamlaka ya Poli hilo lakini cha kusikitisha wamerudisha ng’ombe 47 na ndama 4 kwa maelezo ya kwamba ng’ombe wengine walikufa.
Kufuatia maelezo hayo Mhe. Waziri Mpina alimuagiza Mganga Mkuu wa Wizara na Mwanasheria wa Wizara hiyo kubaki Itilima na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mhe. Benson Kilangi kumwita Meneja wa Poli la akiba la Maswa, Mwenyekiti wa Wafugaji pamoja na wafugaji wanne waliyo taifishiwa ng’ombe zao na nyaraka zao zote, kukutana kesho chini ya uwenyekiti Mhe. Kilangi kujadili suala hili kwa kuzingatia sheria za mifugo na Maamuzi yaliyo tolewa na Mahakama na Waziri apewe mrejesho ili ajue pakuanzia na haki iweze kupatikana
Sekta ya mifugo nimiongoni mwa sekta muhimu sana kuelekea uchumi wa viwanda lakini changamoto lukuki zinazo ikabili sekta hii, ikiwemo magonjwa, uhaba wa malisho, migogoro ya Wakulima na wafugaji, ufugaji usiyo zingatia utaalamu na uwekezaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo, imepelekea sekta hii kudumaa na kuendeshwa bila tija na wafugaji wenyewe kuishi katika maisha ya umaskini mkubwa.
DED - ITILIMA
Sanduku la Posta: 308 BARIADI
Simu: +255 28 29 863 29
Simu: 028 29 863 28
Barua Pepe: info@itilimadc.go.tz
Hatimiliki ©2016 Kitengo cha TEHAMA. Haki Zote Zimehifadhiwa