Wafugaji Mkoani Simiyu wanatarajia kuboresha ufugaji wao kupitia Mpango Mkakati wa kuboresha ng’ombe wa asili kwa njia ya uhimilishaji kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya mifugo, mpango unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Desemba, 2018.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha Wadau wa Mifugo mkoani Simiyu, kilichofanyika Oktoba 10, 2018 mjini Bariadi, kwa lengo la kujadili Utekelezaji wa Mpango mkakati wa kuboresha mifugo kwa njia ya Uhimilishaji (Artificial Insermination),chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.
Akizungumza katika kikao hicho Mratibu wa Mpango wa Uhimilishaji kutoka Shirika la Land O’ Lakes, Bw. Joachim Balakana amesema shirika hilo kwa kushirikiana na mkoa wa Simiyu limelenga kuhakikisha wafugaji wa ng’ombe wa kienyeji na kisasa wanafanya uhimilishaji ili kuboresha mbari za ng’ombe wao na kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa na nyama.
“Uhimilishaji utafanyika kwa kutumia mbegu bora zilizozalishwa hapa nchini katika kituo cha Uhimilishaji Arusha, baada ya ng’ombe wa kienyeji kuhimilishwa tunategemea kupata ng’ombe chotara wa waziwa ambao watakuwa wakitoa maziwa mengi na wa nyama watakaofikia uzito mkubwa ndani ya muda mfupi”alisema Balakana.
Ameongeza kuwa kupitia mpango huu ng’ombe zaidi ya 12,000 wanatarajiwa kuhimilishwa mkoani Simiyu kuanzia Desemba, 2018, huku akibanisha kuwa kutokana na mwitikio mkubwa wa wafugaji na viongozi mkoani humo, ng’ombe zaidi ya hao waliolengwa wanaweza kuhimilishwa na ndani ya muda mfupi matokeo makubwa yakaonekana.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi,Mhe. Festo Kiswaga akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa huo una ng’ombe wengi hivyo, uhimilishaji utasaidia kuongeza thamani ya mifugo kwa upatikanaji wa mbegu bora, ambapo ng’ombe wa nyama watakuwa na uzito mkubwa wakiwa na umri mdogo, ngombe wa maziwa kutoa maziwa mengi na ngozi bora pia itapatikana.
Ameongeza kuwa mkoa huo umejipanga kuboresha ufugaji na kuwasaidia wafugaji kuona thamani ya ufugaji, huku akibainisha kuwa upo uhakika wa kuyaongezea thamani mazao ya mifugo hususani maziwa, kutokana na uwepo wa kiwanda cha maziwa wilayani Meatu ambacho kiko katika mpango wa kupanuliwa ili kukiongezea uwezo katika uzalishaji.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya uboreshaji mifugo ya mkoa wa Simiyu, Katibu Tawala Msaidizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Gamitwe Mahaza amesema jumla ya ng’ombe 348 waliozaliwa kwa njia ya uhimilishaji kati ya ng’ombe 1,598,935 waliopo, hivyo mkoa unaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhimiza uhimilishaji katika halmashauri zote mkoani humo.
Dkt. Gamitwe ametaja moja ya juhudi hizo kuwa ni pamoja na kuzielekeza Halmashauri kutenga asilimia 15 ya mapato ya ndani yatokanayo na mifugo kwa lengo la kuanzisha mfuko wa maendeleo wa mifugo, kuzihamasisha halmashauri kununua vifaa vya uhimilishaji na kununua madume bora.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa wafugaji na wafugaji wamesema wameupongeza uongozi wa mkoa kwa kufikiri namna ya kuboresha ufugaji kupitia na mpango wa uhimilishaji na wakaeleza kuwa wameupokea mpango huo na kuomba uanze kutekelezwa mara moja ili waweze kuona tija katika ufugaji wao.
“Naishukuru Serikali kuleta mpango huu wa kuhimilisha ng’ombe wetu nimeupokea kwa furaha sana na ninaomba wataalam waje haraka kutuelimisha wafugaji, ili uanze kutekelezwa haraka tupate kuona faida ya ufugaji, tupate maziwa mengi na ng’ombe wa nyama wenye uzito mkuwa kama mtaalam alivyotueleza” alisema Bw. Mathias Gabriel Mfugaji kutoka Kijiji cha Mwanegele wilayani Maswa.
“ Nimeupenda mpango wa uhimilishaji ambao utasaidia kuboresha ng’ombe wa kienyeji tulionao sasa, na mimi kama Katibu wa Wafugaji Itilima napendekeza mpango huu utakapoanza uanzie kwangu, ili wafugaji wengine waje wajifunze kutoka kwangu” Katibu wa Wafugaji Wilaya ya Itilima, Samson Kingi Guma alieleza.
Mpango mkakati wa uboreshaji wa mifugo kwa njia ya Uhimilishaji Mkoani Simiyu unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo, Shirika la Land O’ Lakes chini ya Mradi wa Ushirikishwaji wa Sekta ya Umma na binafsi katika utoaji wa huduma za Uhimilishaji (PAID), kwa ufadhili wa Mfuko wa wakfu wa Bill na Melinda Gates.
MWISHO
DED - ITILIMA
Sanduku la Posta: 308 BARIADI
Simu: +255 28 29 863 29
Simu: 028 29 863 28
Barua Pepe: info@itilimadc.go.tz
Hatimiliki ©2016 Kitengo cha TEHAMA. Haki Zote Zimehifadhiwa