Na Haruna Taratibu
Wajumbe wa kamati ya fedha wakikagua jengo la utawala ambapo lipo katika awamu ya tatu ya utekelezaji wake
|
Kamati ya fedha, utawala na mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imeridhishwa na utekelezaji wa Miradi ya maendeleo Wilayani humo, baada ya kufanya ziara katika baadhi ya Miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na Ofisi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri wilayani humo.
Kamati hiyo ilianza Ziara yake katika Mradi wa Jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima awamu ya tatu ambapo ujenzi huo upo katika hatua za ukamilishaji.
Aidha wajumbe wa Kamati walikagua ofisi za jengo hilo, Mfumo wa LAN pamoja na ukumbi mdogo (Maktaba) katika awamu ya tatu ya ujenzi ambao hutatumika kutolea mafunzo na huduma za Kompyuta.
Hata hivyo Mhe. Mwenyekiti wa Kamati na Diwani wa Kata ya Sawida Mhe. Daudi Nyalamo alipendekeza vitengwe vyumba viwili vitakavyo tumika kama vyumba vya kubadilishia nguo kwa Wah. Madiwani Wanawake na Wanaume.
Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkurugenzi sasa upo katika awamu ya tatu ya ukamilishwaji na utakuwa umeigharimu serikali zaidi ya Tsh. Bilioni 1.9 kwa awamu zote tatu.
Wajumbe wa kamati ya fedha wakimsikiliza Mhandisi wa Ujenzi Mkoa (hayupo pichani) akitoa maelezo kuhusiana na mradi wa Bweni la wasichana katika shule ya sekondari Itilima
Kamati ikiwa katika Shule ya Sekondari Itilima wajumbe wa kamati ya Fedha waliambatana Mhandisi wa Ujenzi Mkoa Inj. Mashaka Luhamba kwa lengo kukagua matumizi halisi ya Fedha katika Ujenzi wa jengo la Bweni la wasichana ambalo linajengwa kwa gharama ya tsh. Milioni 80, kutoka serikali kuu na ujenzi huo mpaka sasa upo katika hatua ya ukamilishaji.
Aidha Inj. Luhamba baada ya kutathmini jengo hilo na kujiridhisha alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Bi. Elizabeth Gumbo kwa hatua iliyofikiwa katika mradi huo kulingana na fedha zilizotolewa za ukamilishaji wa mradi huo.
“ili kukamilisha mradi huu makisio ya gharama za ujenzi kwa mujibu wa michoro ni takribani Tsh. milioni 149 na mradi kama huu, ipo katika maeneo mbalimbali, mfano katika Shule ya Sekondari Simiyu iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi walitengewa kiasi kama hiki cha fedha na mradi haujakamilika mpaka sasa” alisema Inj. Luhamba.
Akijibu hoja ya kutotumika kwa nguvukazi ya Wananchi kutoka kwa mjumbe wa kamati hiyo na Diwani wa Viti Maalumu Mhe. SIlya Masebo, Mkurugenzi Mtendaji Bi. Gumbo alisema
“Wakati ujenzi huu unaanza ulikumbwa na changamoto nyingi sana ikiwemo kutokuwepo kwa Wahe. Madiwani kwa hiyo uhamasishaji wa nguvu kazi haukwepo hata hivyo kwa upande mwingine wananchi walikuwa wamebanwa na shughuli za ujenzi wa madarasa hivyo kuleta ugumu wakuwataka ushiriki wao katika ujenzi wa bweni ambalo lilikuwa likihitajika kukamilika kwa haraka”
Mradi huu wa ujenzi wa Bweni katika shule ya Sekondari Itilima ulipata fursa ya kutembelewa na Naibu waziri wa Tamisemi Mhe. David Silinde mwanzoni mwa mwezi Machi na kutaka ukamilike tarehe 30.04.2021.
Wajumbe wa kamati ya fedha wakikagua ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari Madilana.
Kamati ya fedha ilijielekeza katika kata ya Mhuze na kukagua ,miradi miwili ya maendeleo ukiwemo mradi wa ujenzi wa Chumba kimoja cha Maabara katika shule ya Sekondari Madilana na Mradi wa Madarasa Matano (5) , ofisi, matundu matano ya Vyoo katika shule Shikizi ya Ngando.
Aidha wakiwa katika shule ya Sekondari Madilana kukagua mradi wa chumba cha maabara unaotekelezwa kwa fedha kiasi cha Tsh. Milioni 30 wajumbe wa Kamati ya fedha, utawala na mipango wamepongeza kasi ya Mradi, ambapo mpaka sasa sehemu iliobaki ni usimikaji wa Mifumo ya Gesi na katika hili kamati ilishauli malipo ya fanyike baada ya shughuri hiyo kukamilika.
Hata hivyo wajumbe walionyeshwa mradi wa ujenzi vyumba viwili vya madarasa yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi ambapo ujenzi katika hatua ya boma umekamiika bado kupauliwa.
Wajumbe wa kamati ya fedha wakikagua Mradi ujenzi wa Madarasa matano katika shule ya Msingi Ngando katika kata ya Mhunze
|
Kamati ikiwa Katika shule Msingi Ngando katika kata ya Mhunze walikagua mradi wa ujenzi wa Vyumba vitano vya madarasa, ofisi moja na matundu 5 ya vyoo, Mradi uliyotekelezwa na nguvu ya wananchi mpaka hatua maboma na ukamilishaji umetekelezwa na mfuko wa jimbo.
Aidha ilishauliwa na Mthibiti Ubora wa Elimu Itilima Ndg. Steven Simba ili shule hiyo ifunguliwe inapaswa mbao za kuandikia zipakwe rangi, madarasa yawekewe sakafu, Darasa moja litakuwa kama ofisi ya Walimu, vyoo vikamilishwe, lijengwe jiko na uandaliwe muhtasari wa kukiri kuwa eneo la shule hiyo halina migogoro.
Hata hivyo kwa upande wa mradi wa mwanzo uliyo fadhiliwa na Equip wa madarasa mawili, ofisi na vyoo viwili wenye thamani ya Tsh. Milioni 60, kamati ilishauli mradi upakwe rangi upya kutokana na rangi iliyopo kupauka ndani ya kipindi kifupi tangu mradi kukabidhiwa.
Shule ya Msingi Ngando yenye walimu wawili na wanafunzi 278, ikifunguliwa rasmi itapunguza kwa kiasi kikubwa wingi wa wanafunzi katika shule Mama ya Mhunze yenye wanafunzi wasiopungua 2000.
Wajumbe wa kamati ya fedha wakikagua Miundombinu ya Mradi wa Maji katika kata ya migato |
Kamati ikiwa katika kata ya Migato ilipata fursa ya Kukaguwa mradi wa Maji ya bomba wenye thamani ya tsh. Million 153, ambao mpaka sasa umeshakamilika kwa asilimia 100 na kuhusisha ujenzi wa Tanki, nyumba ya mitambo (pump house) na vituo vitano vya usambazaji maji.Akiotoa maelezo kuhusiana na mradi huo meneja wa Ruwasa-Itilima Inj. Banda Issa aliema.
“kwa ujumla mradi huu umeshakamilika na tutaukabidhi kwa jumuhiya ya Watumia maji ngazi ya jamii ili wauendeshe na tunashauli viogozi wetu hususani Wahe. Madiwani watusaidie kuhamasisha jamii wavute maji majumbani kwani taratibu zipo wazi na mchakato wake ni rahisi"
Akijibu hoja ya Mhe. Diwani wa kata ya Migato Mhe. Mbuga Ntobi ya maji kuto patikana kwa kipindi kirefu, Inj. Banda alisema dharula hii ilitonana na ubadirishaji Mfumo wa nishati kutoka matumizi ya nishati ya jua na kuanza kutumia umeme ambapo sasa huduma imeboreka zaidi.
Wilaya ya itilima ni miongoni mwa wilaya zilizo fanya vizuri katika sekta ya maji, miaka mitano kabla hali ya upatikanati maji ilikuwa haizidi 40% lakini katika kipindi cha 2015-2021sa upatikanaji wa maji safi na salama ni zaidi ya 62% hali hii imetokana na dhamira ya dhati ya serikali ya kuhakikisha inasogeza huduma muhumu karibu na jamii ikiwemo huduma ya maji.
Wajumbe wakamati ya fedha, utawala na mipango wakikagua kituo cha kuchotea maji kilichopo katika shule ya msingi Migato |
Kamati ya Fedha ilihitimisha ziara hiyo kwa kukagua mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Wodi tatu katika hospitali ya wilaya ya Itilima ambapo mradi huo unatekelezwa baada ya Halmashauri kupokea kiasi cha Tsh. Milioni 500 kutoka serikali kuu.
Maradi huu upo katika hatua za awali za uchimbaji wa msingi na matarajio utakapo kamilika utahusisha uwepo wa Wodi ya Watoto, na Wodi mbili za wagonjwa wa ndani (IPD).Mradi huu utakapokamilika jumla ya fedha zitakazo kuwa zimetumika ni Tsh. Bilioni 2.
DED - ITILIMA
Sanduku la Posta: 308 BARIADI
Simu: +255 28 29 863 29
Simu: 028 29 863 28
Barua Pepe: info@itilimadc.go.tz
Hatimiliki ©2016 Kitengo cha TEHAMA. Haki Zote Zimehifadhiwa