Mkuu wa wilaya ya Itilima katikati akiwasilisha maelekezo ya Serikali katika kikao cha Baraza la Madiwani |
Mkuu wa wilaya ya Itilima Mhe. Benson Kilangi aiagiza Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato na kujiimarisha katika makusanyo kwa lengo la kujitegemea kimapato
Akiongea katika kikao cha Baraza la Madiwani robo ya tatu Mhe. Kilangi alisema
“Kama Halmashauri haina mapato inakufa, tusikubali kuwa na Halmashauri mfu kwa kukosa mapato, nina imani katika vikao vyenu, hata hivi vya baraza na vikao vingine vya kisheria suala la mapato litaendelea kupewa kipaumbele”
tukiishi katika kutegemea ruzuku ya Serikali kwa maana ile ya ndani inamaana sisi ni watoto wasiokuwa, na maana halisi ya Halmashuri ni mamlaka mpito inayoelekea mahali ijitegemee kama serikali,tuwe nauwezo wa kukusanya mapato tukayatumia sisi wenyewe na walengwa wetu ambao ni wananchi, na katika hili tunatakiwa tuwe na muelekeo sahihi ambao ni wa kupanda kimapato na si kushuka.
Aidha, katika suala la utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma bora kwa Wananchi. Mhe. Mkuu wa Wilaya alisema .
“Hakuna sababu ya kujivunia usimamizi mzuri wa miradi na maboresho yanayofanyika kama hayaambatani na utowaji wa huduma bora kwa wananchi iwe katika sekta ya Afya, maji, barabara au huduma nyingine”
Mhe. Kilangi alisisitiza utolewaji wa huduma bora kwa wananchi uendane na huu uboreshaji na kupunguzo malalamiko yasiyo yalazima au mabango wapitapo viongozi wa kitaifa.
Sanjari na hayo, pia Mhe. Kilangi alitolea ufafanuzi juu ya Kauli ya Serikali ya kuwataka viongozi wa serikali za mitaa, vitongoji na Vijiji kurudisha Mihuli.
“hii kauli isipotoshwe na ikaeleweka vibaya kwa walio kuwa viongozi wetu wa Serikali za Vitongoji na Vijiji, hii ni kauli ya Upendo kabisa yenye lengo la kuwaepusha viongozi na matatizo kwa sababu Mhuli kama ulivyo unaweza ukatumika kwa maslahi mazuri na mabaya, na ifahamike hata siku moja serikali haiwezi kuleta maelekezo ya kuwakomoa viongozi wake hata waliopo katika ngazi za chini za uongozi”
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Bi. Elizabeth Gumbo akiwasilisha utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa robo ya tatu katika kikao cha Baraza la Madiwani |
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuri mbalimbali za Halmashauri kwa robo ya tatu katikao cha Baraza la Madiwani Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Bi. Elizabeth M. Gumbo alisema
“Mpaka sasa Halmashauri tuna asilimia 45(%) ya makusanyo ya mapato kwa mwaka 2020/2021 na katika suala la mapato , ningeomba Wah. Madiwani na Watumishi wenzangu tushiriki kwa pamoja katika ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha shughuri mbalimbali za halmashauri kuendelea ikiwemo kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo, shughuli za ofisi katika Kata, Vikao, Posho na Mishahara ya Wah. Madiwani”
Aidha, Bi. Gumbo alimpongeza Diwani wa kata ya Mwamapalala Mhe. Emanuel Lugisa kwa ushirikiano wa dhati anao utoa katika kuhakikisha mapato yanapatikana na kudhibitiwa.
Kuhusiana na Taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ukaguzi uliyofanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2019/2020 Halmashauri ya Wilaya ya Itilima nimiongoni mwa Halmashauri zilizo pata Hati safi, alisema Bi. Gumbo.
Kwa upande wa Miradi ya maendeleo Mkurugenzi Gumbo alimpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha upatikanaji wa miradi, ikiwemo ujenzi wa wodi tatu, wodi ya Wanawake, Wanaume na Watoto katika hospitali ya wilaya ya Itilima kwa gharama ya Tsh. Milioni 500 na kutupatia Tsh. Milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati tatu katika kijiji cha Laini A, Dasina na Nhobora
Kwa upande wa Miradi ya Elimu Halmashauri imepokea fedha kiasi Tshs million 184.4 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari Nkoma, Madarasa manne katika shule ya sekondari Chinamili, madarasa mawili katika shule ya sekondali Inalo na matundu ya vyoo katika shule ya sekondari mahembe.
Kwa upande wa Elimu za Msingi Halmashuri imepokea fedha kiasi cha Tsh.milioni 372.8 Kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule za Msingi Madilana, Mhunze, Sali,Shishani, Ng’wang’wita, Habia, Bumera, Laini A na Mwalushu.
Katika eneo hili Bi. Gumbo aliwaomba Wah. Madiwani na watumishi kushirikiana kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa ufanisi mkubwa na kuweza kutoa huduma iliyo kusudiwa kwa Wananchi.
Aidha Mkurugenzi Gumbo alitambua jitihada zinazofanywa na wananchi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na katika hili kuna baadhi ya Kata zimefanya vizuri na kusababisha shughuli za maendeleo kwenda kwa kasi ya hali ya juu, aliwapongeza Diwani wa Kata ya Mwaswale Mhe. Nyasunga Chandaluwa na Mtendaji wa kata hiyo Ndg. Safari Joseph Masanyiwa kwa uthubutu wao wa kuwahamasisha Wananchi kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo,
Mkurugenzi Mtendaji akikabidhiwa Madawati 260 na Diwani wa Kata ya Mwaswale Mhe. Nyasunga Chandalua yaliyo tengenezwa kwa nguvu za wananchi |
“Mhe Mwenyekiti, wananchi wa Mwaswale wameweza kujenga matundu tisa ya Vyoo katika shule ya msingi Lung’wa kwa nguvu za wananchi, wamejenga shule za Msingi Mpya mbili katika kijiji Mwamalinze na Mwakubija ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule mama ya Mwaswale na wamenikabidhi madawati 260 yaliyo tengenezwa na nguvu za wananchi na madawati haya yameanza kutumika katika shule ya Sekondari Mwaswale na Lung’wa na wameweza kuanzisha ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha Ng’walali na ujenzi unaendelea” alisema Bi. Gumbo.
Kata ya mwaswale iliyopo pembezoni kutoka Makao makuu ya Wilaya ya Itilima imeweza kukusanya mapato kiasi cha zaidi Tsh. Milioni nne na kutokana na mchango huu Mkurugenzi mtendaji alitoa Motisha ya Vyeti vya pongezi kwa Mhe. Diwani na Mtendaji wa Kata hiyo kwa lengo la kutambua mchago wao katika Maendeleo ya Itilima.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe. Njalu D. Silanga aliwapongeza sana TAKUKURU kwa kuwezesha kurudishwa kwa Tsh. Milioni 7.5 katika kijiji cha Longalambogo na Tsh. Milioni 8 huko mwaswale.
Aidha Mhe. Njalu aliipongeza Idara ya elimu kwa utekelezaji mzuri wa miradi na kupelekea Miradi Kuongezeka
“najivunia sana Idara ya Elimu hamjaniangusha na ndiyo maana fedha zinatiririka hii ni kwasababu mnasimamia vizuri endeleeni kukaza buti”
Aidha Mhe. Njalu aliwaasa Wah.Madiwani kujumuika kwa pamoja katika shughuli za maendeleo na kuhakikisha wanaifahamu miradi na fedha zilizotengwa kwa miradi husika na kuwataka kuimarisha WADC kwa kuleta umoja na mshikamano katika kata.
“ni jambo la ajabu anakuja Mwenyekiti wa Halmashauri au Mkurugenzi na kusoma taarifa kubwa na wewe mhe. Diwani Uzifahamu” Alisema Mhe. Njalu
Sanjari na hayo Mhe. Mbunge aliwaasa idara ya Afya kuhakikisha wanaboresha utoaji wa huduma na kutatua kasoro zinazo jitokeza katika sekta hiyo haraka sana.
Kuhusiana na Suala la Ushirika aliwataka watu wa idara ya kilimo na Ushirika kujiandaa kikamirifu kutokana na Msimu wa Pamba kukaribia na Kuhakikisha Amcos zinakuwa na watu Wenye weredi na wenye hofu ya Mungu ili kuepuka migogoro kama iliyojitekeza katika msimu uliopita.
Kwa upande wa Afisa wa Serikali za Mitaa Ndg. Maganga Simon aliipongeza Halmashauri ya Itilima kwa kuwa miongoni mwa Halmashauri sita (6) zilizofanya vizuri na kupata Hati safi.
“Hati safi maana yake ni kwamba Halmashauri ya Itilima imezingatia Miongozo ya Serikali katika kusimamia rasilimali fedha na rasilimali nyingine” alisema Maganga.
Aidha Ndg. Maganga alisema ya kwamba, pamoja na kupata hati safi kuna maelekezo yaliyotolewa kwenye taarifa ya Mdhibiti na Mkakuzi Mkuu wa hesabu za Serikali na kuzitaka halmashauri kufanyia kazi maelekezo hayo kwa lengo la kupata suluhisho la hoja zinazo tukabili.
“Kuazia tarehe 01- 18/06/2021 wenzetu wa CAG watakuwepo katika halmashauri zetu kwa ajili ya kupitia hoja na kuona hoja zinafungwa na katika hili ushirikiano unahitajika kwa wote na Wahe. Madiwani mnafursa ya kuhakikisha hoja zinafungwa kupitia katika vikao vya kisheria Kuanzia Kamati ya uongozi ya Halmashauri (CMT), kamati ya Fedha, Utawala na Mipango na kutakuwa na Baraza maalumu la Hoja na Mgeni rasmi atakuwa Mkuu wetu wa Mkoa, Mhe. Anthony Mtaka” alisema Maganga.
Aidha Maganga aliipongeza Halmashauri ya Itilima kwa kupeleka zaidi ya asilimia 50 (%) ya mapato ya ndani katika shughuli za maendeleo na kuvuka lengo lililowekwa na Serikali la kutenga asilimia 40 (%) ya mapato ya ndani kwenda katika shughuli hizo.
Diwani wa Kata ya Mwaswale Mhe. Nyasunga Chandaluwa wakwanza kushoto na Mtendaji wake wa Kata Ndg. Joseph Safari wakipokea Vyeti vya Pongezi kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Itilima kama ishara ya kutambua utendaji wao wa kazi uliotukuka |
DED - ITILIMA
Sanduku la Posta: 308 BARIADI
Simu: +255 28 29 863 29
Simu: 028 29 863 28
Barua Pepe: info@itilimadc.go.tz
Hatimiliki ©2016 Kitengo cha TEHAMA. Haki Zote Zimehifadhiwa